TTCL YAZINDUA T-FIBER TRIPLE HUB HUDUMA TATU KWA KIFURUSHI KIMOJA
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi kifurushi kipya cha kidijitali kinachoitwa T-Fiber Triple Hub, ambacho kinajumuisha huduma tatu muhimu katika kifurushi kimoja — intaneti ya kasi isiyo na kikomo, huduma ya simu ya mezani, na huduma ya intaneti pamoja na dakika kwa simu ya mkononi.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya TTCL, na umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa Masoko wa TTCL, Bi. Janeth Maeda, alisema huduma hiyo mpya inalenga kurahisisha maisha ya Watanzania kwa kuwapa huduma zote muhimu za mawasiliano kupitia bili moja tu.
“Dunia ya sasa inaendeshwa na teknolojia. Kupitia T-Fiber Triple Hub, TTCL inaleta suluhisho la kisasa litakalowezesha familia, biashara ndogo na kubwa, pamoja na taasisi mbalimbali kupata huduma bora, za uhakika na zenye gharama nafuu,” alisema Bi. Maeda.
Kwa mujibu wa TTCL, wateja wataweza kupata huduma hiyo kwa gharama kuanzia Shilingi 70,000 kwa mwezi, ambapo watapata intaneti ya kasi hadi 20 Mbps (kupakia na kupakua), dakika 300 za mawasiliano ya mezani, pamoja na GB 20 za intaneti kwa simu ya mkononi.
Kifurushi hicho kinatajwa kuwa na urahisi wa kipekee kwani mteja anaweza kufurahia huduma tatu kwa pamoja kupitia miundombinu imara ya shirika hilo.
TTCL imesema kuwa uzinduzi wa T-Fiber Triple Hub ni sehemu ya mkakati wake wa kuunga mkono ajenda ya serikali katika kukuza matumizi ya TEHAMA na kuunganisha Watanzania katika uchumi wa kidijitali.
“Tunawaalika Watanzania wote kujiunga nasi katika hatua hii mpya ya ubora, urahisi na thamani kupitia T-Fiber Triple Hub,” alihitimisha Bi. Maeda.

Maoni
Chapisha Maoni