TANZANIA NA ZIMBABWE KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI
Tanzania na Zimbabwe zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika nyanja za siasa, uchumi, ulinzi na usalama, biashara, kilimo, elimu, utalii na maendeleo ya kijamii. Hatua hii inalenga kuhakikisha wananchi wa mataifa haya mawili wananufaika moja kwa moja na uhusiano wa kihistoria uliojengeka tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Makubaliano hayo yalibainishwa wakati wa mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Prof. Dkt. Amon Murwira, pembezoni mwa Mkutano wa 22 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Nordic uliofanyika mjini Victoria Falls tarehe 2 na 3 oktoba 2025.
Waziri Kombo alisisitiza kuwa mshikamano wa Tanzania na Zimbabwe umejengwa juu ya msingi wa ukombozi na mshikamano wa kiafrika, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha uhusiano huo unazidi kuimarika. Aidha, aliipongeza Zimbabwe kwa mshikamano wake na Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, akibainisha kuwa mshikamano huo umechangia amani na maendeleo ya kikanda.
Katika kuimarisha diplomasia ya uchumi, Waziri Kombo alisisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta ya utalii, akitolea mfano kivutio cha Victoria Falls na kueleza mpango w
a kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Zanzibar na Victoria Falls ili kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha biashara. Vilevile, alibainisha mafanikio ya ushirikiano wa anga kati ya Tanzania na Zimbabwe kupitia makubaliano ya BASA, ambapo ATCL na Shirika la Ndege la Zimbabwe yanaendesha safari za moja kwa moja zinazochochea utalii na biashara.
Waziri Kombo pia aliipongeza Zimbabwe kwa mshikamano wake katika jitihada za Tanzania kugombea kiti cha Ujumbe Usio wa Kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2027–2028, sambamba na kuunga mkono mapendekezo ya Tanzania kuhusu kuanzishwa kwa Kituo cha Urithi wa Afrika. Aidha, alitolea mfano ziara ya kampuni 16 kutoka Tanzania zilizotembelea Zimbabwe hivi karibuni kwa mazungumzo ya uwekezaji kama kielelezo cha mshikamano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Prof. Dkt. Murwira alisema Zimbabwe inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za ukombozi na itaendelea kudumisha mshikamano huo wa kihistoria na kidugu. Aliahidi kuwa Zimbabwe itaunga mkono jitihada za Tanzania katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, akibainisha kuwa mshikamano huu ni chachu ya kuimarisha mshikamano na kupaza sauti zao katika masuala ya kimataifa.
Uhusiano huo kati ya Tanzania na Zimbabwe unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kuongeza uwekezaji, kukuza ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi wa mataifa haya mawili.



Maoni
Chapisha Maoni