JEMA AFRICA WAZINDUA MFUMO WA ZABUNI WA UNUNUZI WA MAGARI WA MOJA KWA MOJA MTANDAONI 
Na Mwandishi wetu
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Kampuni ya JEMA AUTO, Bw. Lazaro Lutobeka, alisema mfumo huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya kidigitali yanayolenga kurahisisha upatikanaji wa magari moja kwa moja kutoka Japan kwa uwazi, uharaka na gharama nafuu.
“Mfumo huu wa mnada wa magari mtandaoni ni wa kwanza wa aina yake nchini. Unamwezesha mnunuzi kushiriki moja kwa moja kwenye mnada halisi wa magari unaofanyika Japan kwa wakati huo huo, bila haja ya kusafiri. Ni mageuzi makubwa yanayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na ushindani wa haki kwa wateja wetu,” alisema Bw. Lutobeka.
Kwa mujibu wa Bw. Lutobeka, mfumo huu umeunganishwa na zaidi ya minada mikubwa 40 ya magari nchini Japan, na kupitia tovuti ya kampuni hiyo www.jemaauto.com, wateja sasa wanaweza kufikia magari zaidi ya 400,000 yaliyoko tayari kwa mauzo.
Alisema mfumo huo unawezesha washiriki kuweka zabuni zao moja kwa moja kupitia kivinjari cha wavuti au programu ya simu, huku mnada ukionyesha bei za wakati halisi, muda uliosalia na mteja anayeshinda.
Bw. Lutobeka alifafanua kuwa mfumo huo unakuja na manufaa lukuki kwa wanunuzi. Kwanza, unamwezesha mteja kununua kutoka popote duniani bila kuingia gharama za usafiri au malazi, mradi tu ana intaneti na kifaa cha kielektroniki kama simu au kompyuta. Pia unatoa wigo mpana wa magari kuliko kampuni moja, jambo linalompa mteja fursa kubwa zaidi ya kuchagua gari analolitaka kwa bei shindani.
Aidha, mfumo huu unaongeza uwazi wa ushindani kwa kuwa mnunuzi anaona zabuni za washiriki wengine kwa muda halisi, hali inayoongeza uadilifu na kuondoa mazungumzo ya siri. Bei halisi ya soko inaonekana wazi, hivyo mnunuzi anaweza kupata gari kwa bei nafuu kulingana na ushindani uliopo kwa wakati huo.
Vilevile, mfumo unatoa taarifa kamili za gari husika kabla ya mnada kama historia ya matengenezo, idadi ya wamiliki na ubora wa gari kupitia ripoti maalum ya ukaguzi (auction sheet). Mteja pia anaweza kufuatilia kwa urahisi mwenendo wa mnada kwa kuona bei, muda uliosalia na hali ya ushindani wa kila gari bila usumbufu wa mikutano au msongamano wa watu.
Katika hatua nyingine, Bw. Lutobeka alitangaza kampeni maalum ya kumaliza mwaka ambayo JEMA AUTO imeandaa kwa ajili ya kuwazawadia wateja wake wote watakaonunua magari kupitia mfumo huo kuanzia leo hadi Desemba 31, 2025. Kupitia kampeni hiyo, kila mteja atapokea zawadi ya TZS 200,000 taslimu kwa kila gari atakalolinunua.
“Tunataka wateja wetu waone thamani ya kuwa nasi. Hivyo mbali na punguzo hili, mwakani tutaendelea kutoa zawadi kama simu za mkononi, laptop na mabegi maalum kwa wateja watakaokuwa wamenunua magari mengi zaidi katika kipindi hiki,” alisema Lutobeka.
Akielezea kwa nini wateja wanapaswa kuichagua JEMA AUTO, Lutobeka alisema kampuni hiyo ni ya kizawa, inayoaminika na inayotoa huduma kwa uwazi, ubora na bei rafiki. Alisisitiza kuwa magari yote yanayoagizwa kupitia JEMA AUTO yanakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na TBS, yakianzia daraja la ubora wa grade 3.5 na kuendelea.
Pia alibainisha kuwa kampuni hiyo inatoa fursa ya kulipia gari kidogo kidogo, kusafirisha kwa haraka, na kumjulisha mteja kila hatua tangu anaponunua hadi anapokabidhiwa gari lake.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania ana nafasi ya kupata gari bora, kwa bei nafuu na kwa uwazi mkubwa zaidi kupitia teknolojia ya kisasa,” alihitimisha Lutobeka

Maoni
Chapisha Maoni