TLS KUTOA HUDUMA ZA UTETEZI BILA MALIPO KWA WANAOTUHUMIWA KUFANYA VURUGU KIPINDI CHA UCHAGUZI
Chama cha mawakili Tanganyika (TLS) wametoa msaada wa kisheria bila malipo wala masharti yeyote kwa watuhumiwa wote waliofikishwa na watakaoendelea kufikishwa mahakamani katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania baada ya Uchaguzi mkuu ili kuwawakilisha makahamani,kuwatembelea magerezani na kwenye vituo vya Polisi
Akizungumza leo 11 Novemba 2025 na waandishi wa habari Posta Jijini Dar es salaam Wakili wa Mahakama kuu Maduhu William amesema kuwa Tarehe 7 Novemba walianza kuona watuhumiwa mbalimbali wakifikishwa mahakamani kwa makosa ya uhaini,unyang'anyi wa kutumia silaha,uharibifu wa mali,kufanya fujo na makosa ya kula njama.
"Jumla ya Watuhumiwa wa makosa hayo ni 641 mpaka leo wamekwisha fikishwa katika mahakama mbalimbali kote nchini na makosa takribani yote hayana dhamana na kwa mujibu wa sheria ya nchi yetu uhaini na na makosa mengine hayadhaminiki hivyo baada ya mashtaka kusomwa mahakamani Watuhumiwa wote walipelekwa mahabusu na adhabu ya juu ambayo wanaweza kupewa endapo watakutwa na hatia ni kunyongwa hadi kufa na adhabu inayofuatia ni kifungo cha jela maisha na adhabu ya chini kabisa ni kifungo cha jela miaka 30",Maduhu ameeleza.
Aidha Maduhu amesema kutokana na uzito wa adhabu hizo wanahaidi kutoa huduma ya utetezi inayostahili na kwa ukamilifu wake.
"Watuhumiwa wengi ni vijana wadogo kati ya miaka 19 mpaka 25 baada ya mashauri hayo kuanza kufunguliwa tulikaa na kufanya tathmini ambapo tulibaini kuwa watuhumiwa walio wengi uelewa wao wa kisheria ni mdogo na wengi hawana hata uwezo wa kulipia gharama za mawakili kwa ajili ya kuwakilishwa kwa mujibu wa ibara ya 13 ibara ndogo ya sita A ya katiba ya Tanzania ya Mwaka 1977",amesema Wakili Maduhu .
Hata hivyo Maduhu amethibitisha kuwa baadhi yao wamefikishwa Mahakamani na baadhi bado hawajafikishwa na wanaendelea kushikiliwa katika mahabusu na vituo mbalimbali vya Polisi.
"Makundi ya Watuhumiwa Yapo ya aina tatu,kundi la kwanza lilishikiliwa kabla ya tarehe 29 kwa maana tarehe 1 mpaka 28 Octoba,kundi la pili lilishikiliwa siku ya Uchaguzi wenyewe na kundi la mwisho ni kundi lililokamatwa baada ya Uchaguzi kwa maana tarehe 30,31 na kuendelea", amethibitisha
Maduhu amesema "Tumetembelea baadhi yao katika vituo mbalimbali vya Polisi na tumeshuhudia mamia ya vijana wakiwa wamejazana katika vituo hivyo.Kwa hiyo tumebaini kwamba kuna baadhi ya watu ambao wanaendelea kushikiliwa sisi kama mawakili hatukulala nyumbani tuliwatembelea katika vituo vya Polisi ikiwemo Oysterbay tumeona vijana pale wengi,tumeenda kituo cha Mburahati na kuna Watuhumiwa pale na tumeshuhudia wengine wakifikishwa mahakamani mapema mwishoni mwa Juma lililopita ".
Katika hatua nyingine Wakili Paul Kisabo ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwafikisha mahakamani watu wote wanashikiliwa katika vituo vya Polisi na kama hakuna ushahidi kulingana na upelelezi ameomba waachiwe huru ili wakaendelee na majukumu ya kujenga taifa.
"Mtu anapokaa ndani anakuwa hafanyi kazi maana yake anashindwa kuitumikia taifa lake kwa hiyo ni muhimu wakapewa dhamana au wakaachiwa huru ili waweze kuendelea na majukumu mengine ya kulijenga taifa.Lakini pia tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwaruhusu ndugu,jamaa, marafiki na wazazi kuonana na ndugu zao ambao wanashikiliwa katika vituo mbalimbali ili waweze kuwapatia mahitaji ",amesema Kisabo.
Aidha Kisabo amelitaka Jeshi la Polisi kuwaruhusu mawakili kote nchini kuonana na wateja wao ambao wapo kwenye vituo vya Polisi ili waweze kuwapa msaada wa kisheria.
Kisabo ametoa rai kwa familia ambazo ndugu zao wamefikishwa magerezani waende na vitambulisho kwa sababu ndio utaratibu wa magereza.
"Lakini pia tunatoa wito kwa Mkurugenzi wa mashtaka nchini kutumia Mamlaka yake ya kisheria kwa mujibu wa sheria wa mwenendo wa makosa ya jinai kufuta mashtaka hayo kwa sababu kwa tathmini yetu tunaona kwamba mashtaka haya ambayo yamefungliwa kimsingi tunaona hayana miguu kusimama kisheria",Kisabo ameongeza

Maoni
Chapisha Maoni